Jumanne, 30 Julai 2013

MAENDELEO KWA KIJANA NI ZAIDI YA KUPATA SHAHADA

Na:     Albert Leonce Shimiyu.
 
Vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa, ni muhimili wa nchi yeyote yenye mafanikio, uwekezaji wowote ambao haulengi kuwapa nguvu ni batili. Tumaini la nguvu za kufikiri, kubuni na kushindana kwenye ulimwengu wa utandawazi linaweza kufikiwa na vijana wengi kama wataelimika. Katika karne hii ambayo baadhi ya watu wameibatiza la karne ya waafrika, kwa kiasi kikubwa imetoa fulsa ambazo nchi za kiafrika lazima tuzitumie kijiletea maendeleo. Vijana ndiyo wanapaswa  kuwa  viongozi wa kuzitumia fulsa hizo.
Kwa zaidi ya karne moja, Africa imepoteza fulsa nyingi sababu kubwa ikiwa ni kukosa mahusiano sawia miongoni mwa mataifa ambayo mara nyingi yalijijenga kwa misingi ya uporaji na dhuluma  hivyo kudhohofisha nguvu za vijana kwa kuwapatia elimu ambayo iliwafundisha kujidharau na kudharau asili yao.
Elimu ambayo iliwaandaa kuwa wasifiaji wa maendeleo ya  wengine badala kutafuta yao, elimu iliyowaandaa kuburuzwa na utamaduni wa kigeni, iliwaandaa kuulimbukia utandawazi na hata kuhama nchini mwao kwenda ughaibuni. Fikra za kuchangamkia fursa zilifinywa kilindini
kwenye dimbwi la udhalimu na mvurugiko wa akili.
Tulishuhudia kila kijana aliyekuwa akipata elimu wakati huo, hatua ya kwanza Ilikuwa ni kujitenga na jamii zao(waafrika), kujitenga na  utamaduni  wao na kujitenga pia hata na maarifa asili na rasilimali asili. Wakapeda kula kuku choma lakini hawakupenda kufuga kuku, wakapenda kula wali kwa kijiko lakini hawakupenda kulima mpunga. Wakatamani starehe bila kikomo lakini hawakutamani kuzitengenezea hizo starehe. Uzungu hutawala badala ya elimu ya kuzalisha.
Kwa kutamani vyao bila kujua au kwa kujua na kuruhusu rasilimali zetu kuporwa,  yakajengeka mahusiano katika msingi wa udhalimu na chuki isiyo na sababu, yaliwezekana kwa sababu miongoni mwa raia wetu na hata viongozi, walikubali na kukumbatia maovu hayo kwa kufanya  yao, hivyo walitusaliti na kugandamiza ule uliopaswa kuwa uhuru wetu.
Kurekebisha baadhi ya udhaifu ni kitu kilicho ndani ya uwezo wetu, hili litafanikiwa endapo tu tutakuwa na ujasiri na uaminifu wa kutosha kukubali kuwajibika kwa makosa yetu na kukataa mtazamo kujiona wahanga na kuwatupia lawama wengine. Kwa bahati mbaya, hali ya ujasili na uaminifu ni sifa ambazo zinaonekana kutothaminiwa siku hizi na vijana.
Ndiyo maana licha ya kuwa ndani ya fursa lukuki kwa sasa vijana ni walalamikaji mahiri,waandamaji wazuri na wapenda starehe na njia za mkato bila kufanyakazi wala kuchangamkia fursa tele zilizopo ndani ya nchi yetu.
Dhana ya kujiona wahanga inatuzuia kutafuta suluhu ya changamoto zinazotukabili. Ni lazima tuishinde tabia hii na tupambane na matatizo yetu uso kwa uso, hiyo ndiyo dhamira kuu ya vijana kuwa darasani na kuelimika. Mtu aliyeelimika hupambana na kuyapatia majibu na siyo kukubali kuwa mhanga.
Kwa wanaofuatilia histori ya afrika mtakubaliana nami kuwa, vijana wa kiafrika waliambiwa wa kufanywa waamini uongo na hadithi-
tupu zilizobuniwa kutoka ndani  na nje ya nchi zao, ili kuvuruga kila kitu kinachohusu sisi ni akina nani,tunapaswa tuweje na nini tunapaswa kufanya ili kuleta maendeleo yenye ustawi wa jamii zetu tulimo.
Mara zote hushindwa kwa sababu matunda na uhalisia hujitangaza wenyewe, kama vile mtu hawezi kuficha madhara yatokanayo na uongo. Historia chungu,dhalimu naya uongo waliyofundishwa vijana  hatimaye ilikuja kugundulika na vijana wa wakati huo( akina Mwalimu Julius Nyerere) wakatafuta majibu ya udhalimu huo kwa kuanzisha vuguvugu la kuwang’oa wadhalimu ambao lilizaa uhuru wa kweli.
Kwa nini vijana wa leo tunashindwa kuung’oa umaskini hata wa wazazi wetu licha ya kwenda shule na kupata shahada lukuki huku tukiwa tumezungukwa  na rasilimali kibao? Tunapotazama mbele, lazima tutambue kwamba uhuru na maendeleo, kama ukombozi, ni hatua kwa hatua na huja  ukiambatana na majukumu mfululizo na siyo kukaa kijiweni na kulalamika. Lazima tujiimarishe kwa kujifunza kwa walio tutangulia  katika Afrika yote ambao walionyesha thamani ya kujitoa sadaka, ujasiri na ustahimilivu wakati wao wa kudai uhuru.
Ni muhimu vijana kutambua leo hii mbinu mpya za kuendeleza mambo yaliyopita zamani imeibuka kwa namna isiyoelezeka, mara nyingi kwa kusingizia kulinda haki za binadamu, misaada ya kigeni, demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa habari na haki za kimataifa.
Pasipo kutathimini na kujitambua vijana wengi wamegeuzwa kuwa waandamaji, wapiga debe na walalamikaji ndani ya nchi zao. Wamegeuka soko adhimu la bidhaa za kieletroniki na waporaji wa uchumi wa familia ili kuendeleza starehe badala ya uzalishaji.
Hawazalishi chochote isipokuwa lawama na kupiga soga na kusubiri bahati nasibu. Nchi inadidimia!
Kama kweli tunataka kuona ustawi wa watanzania  na waafrika wenzetu, vijana ni lazima, lazima tushinde vipingamizi  hivi kwa kuongeza maarifa, ubunifu, kutumia fursa zilizopo, kufanyakazi kwa bidii na kwa makini, kuacha kulalamika, kupambana na wadhalimu, kushirikiana na kujenda nguvu za kuthamini nchi zetu na uzalendo wa kweli.
Matukio ya Picha ni Siku ya Mahafali ya 12 ya Chuo cha Dar es Salaam City College, ambayo yamefanyika 27/7/2013 katika ukumbi wa Temboni, Picha zote Zimeandaliwa kwa Hissani ya Miss Demokrasia Tanzania na Habari Imeandikwa na Mwanafunzi wa Chuo katika Kozi ya Uandishi wa Habari, Mr. Albert Leonce Shimiyu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni